Saturday, March 17, 2012

Jeshi la Majini la Tanzania lafanyakazi na majirani kupiga vita uharamia



Omar alisema sheria za kimataifa zinauelezea uharamia chini ya mapatano mawili makuu – Kifungu nambari 15 cha Mapatano ya Bahari Kuu ya mwaka 1958 na Kifungu cha 101 cha Mapatano ya Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari ya mwaka 1982. Vifungu hivi vinauelezea uharamia kuwa tendo la vurugu, ukamataji wa nguvu na hasara zinazofanya kwa madhumuni ya siri na mabaharia au abiria wa meli binafsi katika bahari kuu dhidi ya meli nyingine.
Katika mahojiano ya pekee kwa mtandao wa habari wa Sabahi huko Dar es Salaam hapo Jumatatu (tarehe 9 Januari), kamanda alisema kuwa juhudi za vita dhidi ya uharamia vimepunguza matukio ya uharamia katika maeneo ya bahari ya Tanzania kutoka matukio 30 mwaka 2006 hadi tisa mwaka 2011.
Sabahi: Vipi unaweza kuelezea jukumu la jeshi lako la majini katika kupambana na maharamia wa Somali?
Maj. Gen. Said Shaaban Omar: Uharamia
umekuwepo ulimwenguni kote kwa miaka mingi; kitendo cha kwanza cha uharamia kiliripotiwa katika karne ya 13. Karibu na hapa petu, uharamia ulichomoza sura yake mbaya miaka michache baada ya kuanguka kwa serikali ya Generali Siad Barre huko Somalia. Tukio hili kwa bahati mbaya mwishowe limepelekea kutokuwepo kwa uongozi.
Hata hivyo, tatizo lilizidishwa na meli za kigeni zilizokuwa zikiwanyanyasa wavuvi wa Kisomali katika maeneo ya bahari yao. Na kama sehemu ya jawabu yao, wavuvi wa Kisomali mara moja moja walianza kuzishambulia meli za uvuvi za kigeni na kudai kulipwa fedha. Mwisho waliona kuwa raha biashara yao hii na mengine yote ni historia, kwa vile uharamia sasa umeondoka katika maeneo ya baharí ya Somalia – na kukaribia India kwa kaskazini na Msumbiji kwa kusini.
Sasa turudi kwenye suala letu. Tatizo la uharamia katika maeneo ya baharí yetu lilianza mwaka 2006, na kuanzia hapo, kitengo chetu cha jeshi la baharini limeishakamata jumla ya maharamia wa Kisomali 25. Tumeieshawakabidhi polisi ili kuchukulia hatua zifaazao ili sheria ichukue mkondo wake.
Mnamo mwaka 2006, tulikuwa na matukio 30 ya uharamia katika maeneo ya bahari yetu ambayo kitengo changu cha jeshi la baharini limeyashughulikia. Habari nzuri ni kuwa matukio yote hayo 30, kitengo kilimudu kulishughulikia tatizo hili kabla hayajatushinda, katika hatua ya maharamia kufikia kuomba fedha kutoka meli walizokuwa wanazishikia visivyo halali kiliweza kuyadhibiti. Bila shaka, matukio hayo 30 ni pamoja na ukamataji na habari tulizopokea katika kitengo chetu cha jeshi la baharini na meli zilizowagundua maharamia hao.
Habari nzuri ni kuwa tangu kuanza kwa kampeni mwaka 2006, matukio ya uharamia yamepungua kutoka 30 hadi tisa mwaka 2011. Kupungua kwa matukio haya ya uharamia katika maeneo ya baharí yetu ni matokeo ya juhudi zetu za kupambana nayo bila huruma.
Lakini hii si kusema kuwa imekuwa rahisi; kinyume chake. Tumekuwa tukishughulikia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na mambo mengine, maharamia wamekuwa wakitumia mbinu kutoka mashambulizi hadi kupanda meli kwa kujificha usiku. Kitu kama hicho kinaweza kusemwa kuhusu matumizi yao ya silaha, kutoka bunduki aina ya AK-47 hadi mashini gani na silaha nyingine nzito. Imetubidi tuende nao sambamba; vinginevyo, ingekuwa tumepoteza vita hii.
Changamoto nyingine ni, bila shaka, linawasilishwa na ukanda wa mwambao, ambao una kilomita 1,440. Hii ni changamoto kubwa kwa watu na vifaa. Si rahisi kulinda eneo kubwa kama hilo.
Sabahi: Ni changamoto gani za kiuchumi katika kupambana na maharamia?
Omar: Tangu kuanza kwa vitendo vya uharamia katika eneo la bahari yetu, kumekuwepo na kiwango kikubwa cha upungufu wa meli kubwa katika bandari za Tanzania, hasa Dar es Salaam. Meli zimezidi kuchukua tahadhari kabla ya kusafiri kuja Tanzania kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uharamia katika maeneo ya bahari zetu. Meli zenye hatua za usalama wa kutosha pekee zinaendeshwa kwenda Tanzania, kumaanisha upunguaji wa uingizaji nchini. Uwekaji wa hatua za ziada za usalama kwenye meli ulisababisha gharama za ziada za uendeshaji kwa meli hizo -- na mwishoni wanaoingiza bidhaa nchini wanalipa hizo gharama.
Kwa ufupi, hili limepelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa tunazoagiza. Mfano mzuri ni kuongezeka kwa bei ya gesi ya majimbani miezi mitatu iliyopita, kulikosababishwa na kushuka sana kwa meli zinazobeba gesi zinazokuja bandari ya Dar es Salaam. Hali hii ilisababishwa na shambulizi lililoshindwa lililofanywa na maharamia wa Somalia kwa meli iliyokuwa imebeba gesi kufikia Dar es Salaam. Tukio hili lilitokea katika maeneo ya bahari ya Tanzania. Kwa bahati nzuri, tulilizima tukio hili mapema.
Sabahi: Ni maeneo gani mengine yameathiriwa na uharamia?
Omar: Sehemu ya sekta ya utalii vile vile imeathiriwa na tatizo la uharamia. Hakuna chochote kinachoelezea kitu hiki kama meli za kifahari za kitalii, meli za kifahari za abiria zinazopeleka watalii kuzunguka ulimwengu. Mwaka 2006 pekee, kulikuwa na meli za aina hiyo 26 zilizozuru Tanzania. Hata hivyo, idadi hii imeshuka na kufikia meli mbili mwaka 2010 na hakukuwa na meli hata moja mwaka 2011. Yote haya yanaweza kuwa yamechangiwa na vitendo vya uharamia.
Maeneo mengine ni pamoja na uwekezaji wa kigeni wanaotafuta gesi na mafuta katika maeneo ya baharí ya Tanzania. Mpaka sasa, kumekuwepo na majaribio ya uharamia kwa meli zinazoendesha utafutaji wa gesi na mafuta sehemu ya kusini ya mwambao wa nchi, karibu na Visiwa vya Mafia. Hata hivyo, katika mara zote mbili, meli zetu za jeshi la majini ziliweza kuwafukuza maharamia, lakini vile vile zilifanya ukamataji saba.
Sabahi: Kumekuwepo na taarifa kuhusu mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanayoendeshwa na Jeshi la Ulinzi la Tanzania (TPDF) na Kikosi cha Ulinzi cha Kenya. Mazoezi haya yamekuwa aina ya ushirikiano katika bahari?
Omar: Tumekuwa na mashirikiano ya karibu na wenzetu wa Kenya katika maeneo yote yanayohusiana na vita dhidi ya uharamia katika maeneo ya bahari yetu. Karibu kila siku tunawasiliana nao, kubadilishana habari kuhusu kile kinachoendelea katika Bahari la Hindi. Daima tulibadilishana habari kila mara kunapokuwepo na sababu za kuaminika kuwa adui wetu wa pamoja amekimbilia upande wa pili, mbali na mipaka ya kisheria. Kwa neno moja tu, maharamia hawana pa kujificha!
Mbali na Kenya, vile vile tumekuwa tukifanyakazi kwa karibu na majeshi ya wenzetu wa eneo la SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika). Pamoja na kuwa na uhusiano wa kikazi wa karibu na wajumbe wa nchi za SADC, TPDF vile vile ina mahusiano mazuri na wajumbe wanne wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki – Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya. Jeshi la majini la Tanzania vile vile limekuwa likifanyakazi kwa karibu na wenzao wa Msumbuji katika eneo la kusini.

No comments: