Sunday, March 25, 2012

CCM yadai Matumizi helikopta Chadema ni ufisadi’
 Waandishi Wetu
WAKATI Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kikiendelea kutumia helikopta katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za wanachama wake.Jana chama hicho kilifanya mikutano mitano katika kata za Leguruki, Makiba, King’ori, Maloloni na Usa River.


Akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari kwenye mikutano iliyofanyika katika vijiji vya Akheri na Patandi, mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema kwa kutumia helikopta, Chadema wanafanya ufisadi kwani wamekuwa wakiwakamua wananchi fedha za uendeshaji wa chama hicho.

Lusinde alibeza matumizi ya helikopta na kusema kwamba ni kufuru kwa vile kila inapokuwa angani, inatumia Sh60 milioni.

Alisema ya kwamba helikopta hiyo kila irukapo angani kwa saa, imekuwa ikitumia kiasi cha Sh2 milioni kitendo ambacho kimekuwa kikitumia fedha zinazochangwa na wafuasi wa Chadema.

Lusinde, alisema kwamba baadhi ya wafuasi wa Chadema wamekuwa wakikamuliwa kwenye mikutano ya hadhara kuchangia gharama za usafiri wa helikopta hiyo wakati hali yao ni ngumu kimaisha.

“Ndugu wananchi ngoja niwapeni siri hawa wenzetu hawana huruma na nyie kabisa, wanawachangisha fedha za helikopta wakati kila ikiruka hewani sh,60 milioni zinawatoka kuweni makini” alisema Lusinde

Kauli ya Lusinde imekuja wakati kukiwa na taarifa za uhakika kwamba CCM kinatafuta uwezekano wa kuwa na helikopta ambayo wataitumia walau kwa siku tatu au nne za mwisho.

Mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyepo kwenye timu ya kampeni aliliambia gazeti hili kuwa: “Helkopta pia ni siasa, si kwa ajili ya kufanya mikutano mingi tu, kwa hiyo na sisi wakubwa wetu wanahangaika ili walau siku tatu au nne za mwisho tuweze kuitumia”.

Katika uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, vyama vya CCM, Chadema na CUF vilitumia helikopta katika kampeni za kuwanadi wagombea wao.

Gazeti lagawisha bure
Katika hatua nyingine, mamia ya nakala za gazeti la kila wiki (jina tunalihifadhi kwa sasa) jana zilikuwa zikigawiwa kwa watu waliofika kwenye mikutano ya kampeni za mgombea wa CCM, Sioi.

Gazeti hilo toleo nambari 177 la Machi 21 – 27, 2012 lina taarifa nyingi zinazohusu uchaguzi wa Arumeru na baadhi yake zinasema; Chadema wakata tamaa, ‘meseji’ za Nassari zanaswa akikiri kushindwa, Chadema waburuzana kortini wakati tahariri yake inasema Chadema waache uhuni Arumeru.

Gazeti hilo liligawanywa bure na maofisa wa CCM kwa wananchi waliofika kwenye mikutano ya King’ori, Patandi – Maji ya Chai na Leguruki na haikuweza kufahamika mara moja sababu za kufanya hivyo.

Mhariri wa gazeti hilo (pia jina tunalihifadhi) alipoulizwa alisema: "Sifahamu chochote kuhusu suala hilo, labda CCM wamenunua nakala nyingi kwa ajili ya kuwagawia watu wao lakini ngoja nifuatilie maana sikuwapo ofisini kwa wiki nzima".Mratibu wa Mkuu wa Operesheni wa Kampeni wa Chadema jimboni Arumeru Mashariki, John Mrema alisema ni dhahiri kwamba gazeti hilo linasambazwa kukichafua chama hicho na kwamba bado wanatafakari hatua za kuchukua.

Imeandaliwa na Neville Meena, Mussa Juma, Peter Saramba na Moses Mashalla.

No comments: