Sunday, March 25, 2012

Nyumba ya Mungu si shwari 
 Hawra Shamte
AGIZO alilolitoa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Khalid Mandya Februari 13 mwaka huu la  kufunga kwa muda shughuli za uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, kwa wakazi wa eneo hilo liligeuka msumari wa moto uliochoma mioyo yao.

Tamko hilo ambalo alilito wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Magadini Wilaya ya Simajiro, lilikuwa ni sawa na kuwahukumu kifo, kwa sababu bwawa hilo ndilo tegemeo kubwa la maisha yao.

Wakazi wa Magadini, kijiji kinachojumuisha vitongoji vya Magadini, Majengo na Korongo si wakulima kwa sababu ardhi yao ni kame.  

Bwawa la Nyumba ya Mungu ndiyo tegemeo lao, kwa kuwa shughuli yao kuu ni uvuvi.  Hawa samaki ndio wanaowapatia unga, mafuta ya taa na mahitaji mengineyo.

“Kama hakuna samaki hata hao ng’ombe na mbuzi tunaochunga hawatusaidii, kwa sababu ni rahisi kupata fedha kutokana na samaki kuliko ng’ombe au mbuzi, hasa kwa sababu siku hizi mifugo ina matatizo mengi, magonjwa yamekuwa mengi na malisho pia yamekuwa haba,” anasema Mzee Raymond Kishia, mkazi wa Korongo.

Maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu yamepungua na sasa hivi samaki wanapatikana kwa shida, wapo kidogo sana na hawana ukubwa waliokuwa nao awali.

Hayo yanasababishwa na mambo mengi, mojawapo ni mabadiliko ya tabia nchi, joto limeongezeka na kuathiri viumbe hai.  Lakini pia kazi ya mikono ya binadamu;  wavuvi kwa tamaa ya kupata samaki wengi wamekuwa wakivua kwa kutumia nyavu ndogondogo (kokoro)na pia kwa kutumia vyandarua, hivyo huvua hata samaki wadogo na mazalia yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Korongo, Daniel Tengelemingi anasema ingawa Serikali imepiga marufuku uvuvi wa kokoro na uvuvi wa mitengo (kutumia vyandarua vyenye ngao), uvuvi huo umekuwa ukiendelea kwa kificho hasa nyakati za usiku.

“Hivi vyandarua vyenye ngao vina sumu, tena imeandikwa kabisa kuwa dawa yake haimaliziki mpaka baada ya miaka mitano au zaidi, lakini hapa wapo baadhi ya wavuvi wanaotumia vyandarua hivi na kutuingizia sumu kwenye bwawa letu,” anasema Tengelemingi.

Je, serikali ya kijiji haifahamu hali hiyo?

“Sisi tuna wasiwasi na Ofisa Uvuvi wetu, kwani wapo watu wanaoendelea na uvuvi nyakati za usiku na taarifa hizi huyu Bwana Samaki wetu anazo, lakini ametulia tuli kama hakuna kinachoendelea,” Tengelemingi anasema.

Aidha tatizo jingine linalodaiwa kuwapo kijijini hapo ni ubabe wa viongozi wake. Viongozi hao  wanadaiwa kuendesha kijiji kidikteta, neno lao ni amri wamejigeuza kuwa ni mahakama na pia wanawaweka ndani watuhumiwa kwa muda wanaotaka.

“Hapa tulipo hatufuati utawala wa Tanzania bali tupo katika Serikali ya Magadini, kwani hakuna demokrasia hapa, neno lao ni amri, wanakamata watu, wanawafungulia mashtaka, wanawafunga au anawapiga faini,” anasema mkazi mwingine wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Lazaro.

Ukosefu wa chakula

Hali ya maisha Magadini si nzuri kwa sababu ya ukosefu wa chakula.  Mkuu wa Wilaya alipotangaza kufungwa Bwawa la Nyumba ya Mungu, wanakijiji walitoa kilio chao kuwa maisha kwao yatakuwa magumu kwa sababu chanzo chao cha mapato kitafungwa.  

Mkuu wa Wilaya aliwaambia kuwa atawapelekea chakula cha msaada baada ya wiki moja, ahadi hiyo hadi sasa haijatekelezwa.

“Hapa kwetu ardhi ni kavu, huwezi kulima kitu hapa, tunaishi mbugani.  Tunaishi kama ndege, tunatoka asubuhi tunakwenda kuhemea, tukipata chakula tunarudi tunduni jioni, na kwa kawaida familia nyingi hapa zinakula mlo mmoja tu,” alieleza Mzee Kishia.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, anasema eneo lake lina kaya 826, lakini hivi sasa wakuu wengi wa kaya hizo wamelazimika kwenda maeneo mengine yenye maziwa na mabwawa kutafuta maisha.

“Familia nyingi hapa sasa zimebaki na watoto tu, baba zao wameondoka hapa kijijini kwenda katika maeneo mengine kutafuta riziki, wakipata fedha kidogo huwatumia watoto wao kwa njia ya Tigopesa au M-pesa,” anasema Tengelemingi.

Naye Mzee Paulo Kipaini anasema kipato cha wananchi wanaoishi kandokando ya Bwawa la Nyumba ya Mungu kimeshuka, hivi sasa wengi wanashindwa hata kulipa ada ya shule ya watoto wao.

“Watoto wetu wamerudishwa nyumbani kutokana na kukosa ada, kwa kawaida tunatakiwa kupeleka shule debe sita za mahindi, debe tatu za maharage na Sh60,000 kwa mwaka, lakini sasa hivi hatuna fedha za kununulia chakula wala hatuna fedha za michango ya shule,” anasema Kipaini.  

Mwadawa Mdee, Mkazi wa Korongo, kijijini Magadini, katika Wilaya ya Simanjiro, anasema maisha kitongojini hapo sasa hivi ni magumu kwa sababu kazi kubwa ya wakazi wa hapo ni uvuvi, lakini sasa Serikali imewakataza kuvua kwa sababu ya uvuvi haramu unaoendelea.

Mwadawa anasema Serikali imefanya vyema kuzuia shughuli za uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa sababu uvuvi unaofanywa, unahatarisha mazingira, lakini hata hivyo, wakazi wa vitongoji vilivyo pembezoni mwa Bwawa la hilo, wameathirika kiuchumi.

“Hali ni ngumu, wanaume wanalazimika kuacha familia zao kwenda maeneo mengine kutafuta maisha.  Kusema kweli maisha yetu yamekuwa ya kubangaiza, ukipata mlo mmoja unashukuru,” Mwadawa anaeleza.

Kauli ya Serikali

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Khalid Mandya,  anasema kuwa ni kweli alifika Magadini Februari 13 mwaka huu na kutoa amri ya kulifunga bwawa hilo na kuahidi kuwapelekea wananchi chakula cha msaada, lakini chakula hicho si kwa sababu ya kufungwa kwa bwawa, bali ni kutokana na ukame uliosababisha uhaba wa chakula ndani ya wilaya tatu ambazo ni Simanjiro, Mwanga na Moshi.

“Kweli tuliahidi kupeleka chakula, lakini si kwasababu ya kufungwa kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu,  bali ni kwa sababu ya uhaba wa chakula uliokabili maeneo hayo.  Chakula cha msaada bado hatujakipeleka kwa sababu bado hakijapatikana, kikipatikana tu tutakipeleka,” anasema Mandya.

Kuhusu tatizo la uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, Mandya anasema wanajipanga kama mkoa wa Kilimanjaro na Manyara kulishughulikia tatizo hilo.

“Tulilifunga bwawa si kwa sababu hatutaki wananchi wavue, bali kwa sababu hakuna cha kuvua, samaki wamekwisha na hata maji ya bwawa yamepungua kutokana na uharibifu wa mazingira, hivyo tunajipanga kukabiliana na tatizo hili la uharibifu wa mazingira kikamilifu kama mikoa.
“Karibuni tutaanzisha doria kali kuzungukia vijiji na vitongoji vyote vilivyo kandokando ya bwawa ili kudhibiti uvuvi haramu,” alieleza Mandya.

Tatizo la maji

Mzee Jeremiah Tengelemingi, anasema Korongo imetengwa, haina maendeleo, mbali na shida hiyo ya chakula hata maji ni shida, hivi sasa wananunua dumu moja la maji kwa Sh700 maji ambayo hutolewa Moshi na kuletwa kijijini kwao kwa baiskeli au pikipiki.

“Maji ya bwawa hatuwezi kuyanywa kwa sababu si salama.  Takataka zote za viwandani zinaingia bwawani na mvua ikinyesha inasomba uchafu wote wa milimani na kutumbukiza bwawani, hivyo hatuwezi kuyanywa maji haya,” anasema Tengelemingi.

Sehemu kubwa ya Bwawa la Nyumba ya Mungu imekauka na hata mvua zilizotarajiwa kunyesha kuanzia katikati ya Machi, hazijanyesha mpaka sasa, hivyo ukame unatishia amani mkoani Kilimanjaro kwani hata wafugaji wanalazimika kupeleka mifugo yao mbali kutafuta malisho.

Hata hivyo si kama Serikali haitambui tatizo la maji katika kijiji cha Magadini na vijiji vinginevyo, kwani Serikali ilishatoa tenda ya kutandaza mabomba kuyafikisha katika vitongoji vyote vya Magadini ili viweze kupata maji, lakini tuhuma zilizopo ni kuwa wajanja wameuhujumu mradi huo kwani wametandaza mabomba mabovu yaliyopasuka.

“Mabomba yametandazwa lakini hayatoi maji kwa sababu ni mabovu, hii ni hujuma ya makusudi na inaonyesha kuwa wako waliofaidika na mradi huu,” alisema Fraiko Kihedu, Katibu wa Kamati ya Kitongoji cha Korongo.

Kihedu, anasema tatizo la Magadini ni kwamba wananchi hawana pahali pa kukimbilia kwenda kueleza kero zao, na mara nyingi uongozi wa kijiji umekuwa ukiwatishia uhai wananchi.

“Uongozi hautaki kukosolewa wala kushauriwa, wanafanya wanavyotaka na wanaamua yale yenye maslahi kwao tu na wala si maslahi kwa wanakijiji,” alidai Kihedu.

Ahadi isiyotekelezeka
Baada ya kuona kuwa madhila yamezidi hasa kwa wakazi wa kitongoji cha Korongo,  wameandika barua kwa kijiji hadi wilayani kuomba Korongo ipewe hadhi ya kijiji kwa sababu inatimiza masharti yote ya kuwa kijiji.

“Hapa Korongo tuna kaya 862, wakati eneo linaweza kuwa kijiji kwa kuwa na kaya 250 tu, ombi hilo limekuwapo kwa zaidi ya miaka 15 sasa lakini halitiliwi maanani,” alisema Kihedu.

Aidha Kihedu anasema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, waliokuwa wakiomba uongozi waliwaahidi wakazi wa Korongo kuwa wakiingia madarakani watahakikisha kuwa Korongo inapewa hadhi ya kijiji, lakini hadi sasa hakuna hata dalili ya wakazi wa Korongo kutekelezewa dai lao hilo.

“Huku Magadini shughuli zinazoingiza kipato ni mchanga na samaki.  Huku kuna machimbo ya mchanga, lakini cha ajabu ni kuwa kipato kitokanacho na mchanga, hakiwanufaishi wananchi.

Mchanga umekuwa ni mradi wa wakubwa, kipato chake hakiakisi katika maendeleo ya kijiji chetu,”  Kihedu alieleza

No comments: