Sitta awashangaa CCM wanamhofia kwa nafasi hiyo
Fidelis Butahe
NAIBU
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Zitto Kabwe
ameibuka na kusema kuwa anataka kuwa rais wa Tanzania mwaka 2015.Wakati
Zitto akitoa kauli hiyo nzito, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta naye amesema anashangazwa na watu wanaoweweseka
wanaposikia kuwa mwanasiasa huyo anayeongoza vita dhidi ya ufisadi
ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, anataka kuwania urais.
Kauli
hiyo ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni huenda ikaibua mjadala mzito
ndani ya chama chake, ukiacha zile mbio za vigogo wa CCM wanaotajwa
kuutaka urais 2015.
Katika taarifa yake aliyoituma jana kwa
gazeti la Mwananchi Jumapili, Zitto alisema; “ Kwanza niseme wazi kabisa
kuwa Urais ninautaka, nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili
changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu
kukabili changamoto hizi.” Alitamba anao uwezo kwa kuwa ni mzalendo,
mwenye utashi wa kuleta mabadiliko stahiki kulingana na nchi
inavyoongozwa. Katika taarifa hiyo ameeleza kuwa kwa sasa nchi
imesahau maendeleo ya watu badala yake imejikita katika maendeleo ya
vitu.
“Ninajua kuwa hivi sasa viongozi wetu wengi wanaangalia
zaidi mitindo badala ya mambo ya msingi,” Zitto amesema taarifa na
kuongeza: “Ninajua kuwa maendeleo vijijini yamesahaulika, ninajua nchi
yetu inahitaji uongozi wa kufanya mabadiliko makubwa badala ya
mabadiliko ya juujuu.”
Alieleza kuwa mabadiliko makubwa
yanahitaji maamuzi magumu yatakayoudhi wengi hasa vigogo wa nchi za
Magharibi huku akitoa mfano kuwa ni pamoja na kuzuia nchi kuuza
malighafi pekee. Alisisitiza kuwa rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa
mali ya umma ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo ya nchi na kwamba lazima
hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi.
“Rasilimali
kama madini, mafuta, gesi asilia, ardhi na nyinginezo ni lazima
zifaidishe wananchi wa nchi yetu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Sababu za kutaka Urais Katika taarifa hiyo Zitto alieleza kuwa kwa
sasa nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto muhimu na
kwamba yeye anaweza kuwaongoza Watanzania kukabiliana na changamoto
hizo. “Sio kazi rahisi, lakini ni kazi ambayo lazima Mtanzania mmoja
aifanye, mimi nataka kuifanya, nina uwezo wa kuifanya,” alitamba katika
taarifa hiyo.
Alieleza kuwa hata kama anaitaka kazi hiyo, ni
lazima Watanzania walio wengi waamue, pia ni lazima Chadema kiseme wazi
kuwa yeye ndio anastahili kuifanya kazi hiyo na kwamba kuitaka tu
nafasi hiyo hakutoshi bila ridhaa hizo. “Kama wananchi watasema huyu
Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema
hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama
hawataki kabisa tuache iwe hivyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Umri wa kugombea urais Katika taarifa hiyo, Zitto alieleza kuwa
mjadala wa umri wa kugombea urais umekuwa mkali na kwamba baadhi ya watu
kwa sababu zao binafsi, wameamua kuuita ni mjadala wake na Mbunge wa
Bumbuli January Makamba ambao unaowabagua wazee.
Alisema
kuwa wakati akisoma Chuo Kikuu Dar es Salaam(UDSM), Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Hai, alimuomba
kushiriki kikamilifu kukijenga chama hicho kutokana na kukimbiwa na
wanachama isipokuwa wale waliokuwa wakitokea Kigoma, Kilimanjaro,
Shinyanga, Karatu na Ukerewe.
“Mwaka 2001 muongo mmoja
uliopita ni mimi na Mbowe ndio tuliofanya mabadiliko yote yanayoonekana
Chadema. Tumeingiza watu wapya na tumeandika Katiba upya, tulichambua
mambo mengi na Mbowe kuijenga Chadema,” alieleza katika taarifa hiyo.
Alieleza kuwa mwaka 2005 Mbowe aligombea urais na kwamba
walijua kuwa watashindwa ila walitaka kukijenga chama hicho na walipata
wabunge na kuongeza kuwa mwaka 2010, Chadema kilishiriki uchaguzi mkuu
kama chama imara kinachokwenda kuchukua dola. Huo ndio ukawa mwanzo wa
kuibuka kwa wabunge John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), wabunge
ambao alieleza kuwa awali walionyesha wasiwasi mkubwa kujiingiza katika
siasa.
“Baadhi ya watu wazima waliingia Chadema kwa sababu ya
vijana, nani anasema hatulei vijana kuwa viongozi wazuri, nani haoni
hazina ya viongozi vijana hivi sasa ndani ya Bunge kutoka vyama vyote.
Kuna namna bora ya kulea viongozi zaidi ya kuwapa majukumu?” Alihoji
katika taarifa hiyo.
Hoja ijadiliwe Katika taarifa hiyo Zitto
alifafanua kuwa hoja ya umri wa kugombea urais iwe na mahali pakuanzia
na inapaswa kujadiliwa bila kuangalia majina ya wanaotetea hoja hiyo.
Suala hilo lijadiliwe kwa faida na hasara zake na kufafanua kuwa hakuna
anayejua kuwa yeye atakuwa hai mwaka 2015 na kwamba isiandikwe katiba
yenye kupanua wigo wa kutoa haki ya kugombea urais kwa sababu yake.
Samuel Sitta
Akizungumza
na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika Tamasha Vyombo vya
Habari lililofanyika jana kwenye Ukumbi Msasanki Beach, Dar es Salaam,
Sitta alieleza kuwa anashangazwa na watu wanaoweweseka wakisikia anataka
kuwania urais mwaka 2015.
"Nashangaa watu wanapata kiwewe
kusikia nataka kuwania urais, kuwania urais ni haki ya kila Mtanzania na
Watanzania ndiyo watakaoamua nani ni mzuri na atawafaa," alisema Sitta
na kushangiliwa na waliohudhuria tamasha hilo.
"2015 tunataka
kuwa na mwelekeo mzuri, nikiwa na maana mambo ya hongo, ubadhirifu
hatutaki yawe na nafasi, alisema Sitta na kuongeza:
"Kuna hadithi
moja, siku moja trafiki mmoja alikamata gari pale Mwenge (Dar es
Salaam) akaomba, leseni, akaangalia kadi ya gari sasa yule mama alikuwa
na mtoto wake ana miaka kama minane, akamwambia mama yake, mpe kitu
kidogo...hivi imefikia hatua hata mtoto wa miaka minane anajua rushwa."
Alisema
rushwa imesababisha nchi kuingia mikataba ya uongo, kuna mikataba mingi
ya uongo na ndio maana leo hii nchi imefika hapa ilipo.
"Hii
imesababisha matatizo hadi ya umeme, tungeweza kuuza umeme wetu nje,
lakini leo haiwezekani, nasema haya kama mzee wenu na kiongozi wenu.
"Sasa,
nawaasa waandishi, msikubali kuwa mawakala wa viongozi waongo,
msikubali uongo na kama tungeendelea kule uongo, nchi
ingeharibika...hatuwezi kusonga mbele kwa uongo na vyombo vyenu
visitumike kusambaza mambo ya uongo," Sitta alishauri.
No comments:
Post a Comment