Sunday, March 25, 2012

Ewura yaingilia mgogoro wa mafuta

 Fidelis Butahe  MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeingilia kati mgogoro ulioibuka katika Kamati ya Kuratibu Uagizaji Mafuta (PIC) kutokana na wajumbe wa kamati hiyo kutoelewana.  Kutokana na mgogoro huo Ewura imeiandikia barua kamati hiyo ikiitaka kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha mradi huo. Katika barua hiyo ya Machi 16, mwaka huu, iliyotiwa saini na Anastas Mbawala kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu inaeleza kuwa mamlaka imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa PIC kuhusu kutoelewana na mwenyekiti wao.   “Miongoni mwa sababu za kutoelewana ni kuhusu usalama wa nishati hiyo na bei ya kununua na kuuza” ilieleza sehemu ya barua hiyo.   Katika barua hiyo, PIC inaelekezwa kufanya ajira ya menejimenti ya kudumu na watumishi wengine.   “Ewura imeliona na kulichukulia suala la ajira ya menejimenti ya kudumu ya PIC na watumishi wengine kuwa la muhimu, lakini limechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa.”,    “Kuendelea kucheleweshwa kwa jambo hilo kunaweza kuathiri ufanisi wa mpango mzima wa kuagiza mafuta kwa pamoja,” ilieleza taarifa hiyo.   Katika barua hiyo Ewura imeielekeza Bodi ya PIC  kuunda menejimenti ya kudumu ndani ya siku saba tangu kuandikwa kwa barua hiyo.  Moja ya mambo yalioamuliwa ili kupunguza bei ya mafuta ni pamoja na kuwa na mpango wa kuagiza mafuta kwa pamoja.  Baadhi ya wafanyabiashara hao wameipongeza serikali hasa Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa na mpango huo kwa kuwa utapunguza baadhi ya gharama.   Gharama zilizopungua ni muda wa meli kusubiri kushusha mafuta bandarini Dar es Salaam. Muda huo umepungua kutoka wastani wa siku 40 mwaka 2011 hadi siku nane hivi sasa.   Bei ya petroli hadi jana nchini ilikuwa Sh2,144 kwa lita na dizeli ilikuwa Sh2,093.   

No comments: