Sunday, March 25, 2012

Unapoamua kupenda, vaa uvumilivu, ikibidi kubali kuwa bwege

 Mada hii ina lengo la kukufanya uyaelewe mapenzi. Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.

Ni sehemu ya tatu. Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huohuo ukawa unajali za kwako. Kwa pamoja ndipo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote.
Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote. Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.
Penda kuamini kuwa “hili nalo litapita” kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.
Ukitaka kulazimisha awe mchangamfu kwako kipindi ambacho amenuna, ni sawa na kukaribisha matatizo zaidi. Ni vema kuelewana, watu wengi wanakosea katika uhusiano wao kwa sababu hawatumii busara ili kuwaelewa wenzi wao pindi wanapoonesha hali tofauti.
Busara iendelee kuchukua nafasi. Maneno “hili nalo litapita” yawe somo kwako. Kwamba leo umerudi nyumbani, umetaka chakula cha faragha, mwenzako amekwambia hajisikii vizuri. Hutakiwi kupandisha mizuka na kusababisha nyumbani pasilalike kwa siku hiyo.
Badala yake unapaswa kuvumilia. Jiulize mmefanya tendo mara ngapi katika uhusiano wenu, iweje siku hiyo akwambie hajisikii? Ukilazimisha ni sawa na kumfanyia mwenzako ubakaji. Si ajabu akiona unakuwa mkali, akakubali kukupa kwa shingo upande lakini si kwa ridhaa yake.
Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi kwa maana nyakati nyingine utalazimika kuvumilia mambo ambayo pengine yakakuumiza. Mpo wawili na kujenga tafsiri ya mwili mmoja. Pengine hata makundi yenu ya damu ni tofauti. Ilivyo maumbile yenu ni hasi na chanya ndiyo na damu zenu zilivyo.
Tofauti hiyo mnaielewa na kuikubali, iweje siku ukirudi nyumbani unamkuta amenuna na hataki kuzungumza na wewe ushindwe kuelewa? Hapo ndipo uvumilivu wako unahitajika. Ni kipindi ambacho busara zako zinapaswa kufanya kazi kwa asilimia 100. Usilazimishe afanye upendavyo wakati mwili wake haupo tayari.
Unaingia faragha na mwenzi wako. Ameshindwa kukuridhisha kabisa. Ni hekima zako kutambua kwamba siku hazilingani. Mbona siku nyingine alikupa mambo mazuri mpaka ukasema ‘poo’? Tatizo ni nini? Pengine nishati za mwili wake kwa siku hiyo hazipo sawasawa na hata yeye mwenyewe hajui.
Ukimkejeli kuwa hajiwezi ni sawa na kumchinjia baharini. Siku zinazokuja atashindwa kabisa. Si kwa sababu uwezo wake ni mdogo, la hasha! Maneno yako ya kejeli na dharau ndivyo vitakavyoufanya moyo wake usinyae na kukuogopa ndani kwa ndani. Fikra zake zitashambuliwa na ugonjwa hatari.
Si ugonjwa unaosababishwa na kirusi, hapana. Ni gonjwa la maneno litakaloshambulia ubongo wake. Kila mara kabla ya kuingia mchezo atakuwa na maswali ya kujiuliza: “Sijui leo nitashindwa tena?” “Nikishindwa itakuwaje?” “Atanitukana tena?”  “Hivi mimi ni mgonjwa?”
Mwisho wa maswali hayo atahitimisha kauli kwa kusema: “Inawezekana mimi ni mgonjwa kweli ndiyo maana nashindwa kazi.”

No comments: